Friday, October 30, 2009

MAUAJI YA WALEMAVU WA NGOZI NCHINI TANZANIA.

WIMBI la mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi hapa nchini linazidi kushika kasi kila kukicha licha ya kuwa serikali inafanyajitihada za kuweza kumaliza tatizo hilo lakini bado jitihada hizo hazijazaa matunda kwani bado mauaji hayo yanazidi kuripotiwa sehemu mbalimbali hapa nchini ambapo hadi kufikia oct 2009 inakadiliwa albino zaidi ya 50 wameripotiwa kuuawa.

CHANZO CHA MAUAJI HAYO:
Katika utafiti uliofanywa na mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali pamoja na serikali walibaini kuwa chanzo cha mauji hayo ni imani za kishirikina ambazo baadhi ya watu wanaamini kuwa ukiwa na nywele za albino ama kiungo chochote cha mwili wa albino na ukakipeleka kwa waganga wa kienyeji utakuwa tajiri. Jambo hili limepelekea mauaji hayo kushika kasi hapa nchini kwani baadhi ya wanaotuhumiwa kusababisha mauaji haya kuongezeka ni wafanyabiashara wa madini,wavuvi na wanasiasa.
Chanzo kingine ni waganga wa kienyeji ama wa jadi ambao wamekuwa wakidaiwa ndiyo wanawatuma watu wawaletee viungo vya mwili wa binadamu ili wawatengenezee wapate utajiri cha kujiuliza ni kwamba kwanini wao wasiwe matajiri wakati uwezo huo wanao hapa inaonyesha ni kwajinsi gani wanachangia wimbi la mauaji kuongezeka na kundi hili ndilo chimbuko la mambo yote kwa kuwa wao ndiyo chanzo kikubwa.

Hata hivyo wale wanaojiita waganga wa tiba asili wanataka watofautishwe na waganga wa kienyeji au jadi. Wanadai kwamba wao wanatumia mitishamba katika matibabu yao na wale wa jadi na kienyeji wanatumia uchawi na viungo vya binadamu kuwaroga maadui wa wateja wao pia kuwazindika wateja wao lakini hata hivyo bado wote wanafanya kazi moja.

Tangu mwishoni mwa mwaka 2008 serikali ya Tanzania imekuwa ikichukua hatua mbali mbali kupambana na mauaji hayo ikiwa ni pamoja na kupiga kura za maoni kuwabaini watu wanao wauwa ,wafanyabiashara wa viungo vya albino,wanunuzi na wanaowatuma.
Kutokana na hatua hiyo serikali imeweza kuwatia hatiani baadhi ya watu wanaotuhumiwa kuhusika ambapo tayari watu watatu wameshahukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya upelelezi kukamilika na kutolewa ushahidi katika mahakama maalum ya Tanzania kituo cha Kahama mkoani Shinyanga huku kesi nyingine kama hiyo iko mbioni kutolewa hukumu katika mahakama kuu ya Tanzania kituo cha Shinyanga baada ya kuwa ushahidi wake umekabilika na waliokutwa na hatia ni watu wanne akiwemo aliyekuwa mwenyekiti wa kijiji cha Nkindwabiye wilaya ya Bariadi Nchenyenye Kishiwa[61] mwenyekiti wa kitongoji cha Isanga Sayi Gamaya[46] Mboje Mawe[50] na Sayi Mafizi[33].

KWA HABARI ZAIDI KUHUSU HUKUMU ILIYOTOLEWA KAHAMA SOMA TAARIFAFA HAPO CHINI.






Watatu kunyongwa kwa kumuua albino
• Maelfu walipuka kushangilia hukumu hiyo

na Stella Ibengwe, Kahama


MAHAKAMA Kuu ya Tanzania kituo cha Kahama, imewahukumu kunyongwa hadi kufa washitakiwa watatu baada ya kupatikana na hatia ya kula njama na kufanya mauaji ya kinyama ya kukusudia dhidi ya mtoto Matatizo Dunia (13), aliyekuwa na ulemavu wa ngozi (Albino).Waliokumbwa na adhabu hiyo ni Masumbuko Madata (32), mkazi wa Itunga, Emmanuel Masangwa (28), mkazi wa Bunyihuna na Charles Kalamuji au Charles Masangwa (42), mkazi wa Kijiji cha Nanda wilayani Bukombe, mkoani Shinyanga.
Akitoa hukumu hiyo ambayo ni ya kwanza tangu kuanza kusikilizwa kesi za mauaji ya albino kituo cha Kahama na Shinyanga, Jaji wa Mahakama Kuu, Gabriel Rwakibalila, alisema mahakama imeridhishwa na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo, kwamba washitakiwa wote watatu walikula njama na kufanya mauaji hayo usiku wa kuamkia Desemba mosi 2008, katika Kijiji cha Bunyihuna, wilayani Bukombe, mkoani Shinyanga.
Mbele ya umati wa watu waliofurika kusikiliza hukumu hiyo ya kihistoria nchini, Jaji Rwakibalila alisema ushahidi wa upande wa utetezi uliotolewa mahakamani hapo, ulionyesha washitakiwa hawakuwepo siku ya tukio, lakini ni utetezi huo huo ulioonyesha kuwa ndio waliokula njama na kufanya mauaji hayo.
Katika hukumu hiyo iliyosomwa kwa takribani saa moja, Jaji Rwakibalila aliendelea kusema pamoja na dosari ndogo zilizoonyeshwa na upande wa serikali, haziwezi kuharibu shitaka lililokuwa likiwakabili washitakiwa hao na kuwatia hatiani.
Alizitaja baadhi ya dosari hizo kuwa ni tofauti ya ushahidi wa idadi ya askari na magari yaliyofika eneo la tukio, lakini alisisitiza kuwa ushahidi huo unatosha kuwatia hatiani washitakiwa hao na kupewa adhabu hiyo kwa mujibu wa sheria ya makosa ya jinai namba 196 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Kuhusu ushahidi wa Mkemia Mkuu wa Serikali, Jaji Rwakibalila alisema unaonyesha kuhusika kwa mshitakiwa wa kwanza na wa tatu katika mauaji hayo hasa baada ya kupatikana kwa vinasaba ambapo damu ya miguu yote miwili ya albino Dunia ilipochukuliwa, iligundulika kuwa na vinasaba hivyo.
Huku akiwa makini kusoma hukumu hiyo, Jaji Rwakibalila aliendelea kusema kuwa ameridhika washitakiwa hao watatu walishiriki katika mauaji hayo na ndiyo maana wametiwa hatiani.
“Mshitakiwa wa kwanza, Masumbuko Madata, mshitakiwa wa pili Emmanuel Masangwa na Charles Kalamuji au Charles Masangwa nyote kwa pamoja mmepatikana na kosa la mauaji, hivyo mahakama inawahukumu kunyongwa hadi kufa na mnaweza kukata rufaa kama hamjaridhika na hukumu hiyo,” alihitimisha kusoma hukumu yake Jaji Rwakibalila huku wananchi waliokuwepo wakionyesha kuifurahia kwa kupiga kelele za kuipongeza serikali.
Mara baada ya hukumu hiyo, washitakiwa hao waliangua kilio wakidai wameonewa, huku ndugu zao wakiungana nao kupaza sauti za kudai haki haikutendeka.
Mawakili wa upande wa utetezi, waliungana na wateja wao kulalamikia hukumu hiyo kuwa imetolewa kwa hasira bila kuzingatia sheria kwani wateja wao hawakuwa na hatia.
Kutokana na hali hiyo, mawakili hao kwa nyakati tofauti walidai wanakusudia kukata rufaa dhidi ya hukumu ya kesi hiyo ya mauaji, namba 24 ya mwaka 2009.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa niaba ya wenzake, kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi, Kamaliza Kayaga alisema hawajaridhika na hukumu hiyo na kusisitiza kuwa watakata rufaa ili wateja wao watendewe haki.
Kesi hiyo iliyokuwa ikivuta hisia za Watanzania wengi, ilianza kusikilizwa Juni 8, mwaka huu.
Upande wa mashitaka katika kesi hiyo, ulipeleka mashahidi 15 wakati washitakiwa walipeleka mashahidi watatu tu.
Katika hatua nyingine kesi nyingine inayohusu mauaji ya bibi kikongwe, aliyeuawa kwa imani za kishirikina.inatarajiwa kutolewa hukumu katika mahakama hiyo Jumatatu.
Wakati huohuo, Mahakama Kuu kituo cha Shinyanga inayosikiliza kesi nyingine ya mauji ya albino, itaanza kusikiliza ushahidi wa upande wa utetezi wa washitakiwa wanne baada ya kubainika kuwa wana kesi ya kujibu.
Washitakiwa hao ambao kesi yao nao ilianza kusikilizwa Juni 8, mwaka huu ni Mboji Mawe (50), Mshenyenye Kisiwa, (50) Sahi Jamaya (47) na Sahi Masizi (56), wanaotuhumiwa kumuua albino Lyaku Willy. Wana kesi ya kujibu.
Kutokana na hali hiyo, kesi hiyo sasa itaanza kusikilizwa mfululizo kesho chini ya Jaji Gad Mmjemasi wa Mahakama Kuu, kituo cha Shinyanga.
Katika kesi hiyo, upande wa mashitaka unatarajia kupeleka mashahidi 14 wakati upande wa utetezi unatarajia kupeleka watatu.
Hii ni mara ya kwanza, mahakama kuwatiani hatiani watuhumiwa wa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi baada ya kilio cha muda mrefu kutoka kwa watu mbalimbali kuishutumu serikali kuwa haichukuwi hatua sahihi dhidi ya wahusika.
Hatua hiyo, ilisababisha serikali kuendesha zoezi la kupiga kura ili kuwabaini wauaji, majambazi na watumia dawa za kulevya zoezi ambalo lilizinduliwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

No comments:

Post a Comment